Semenya hatotetea taji lake la dunia katika mashindano ya Doha

224

Mwanariadha wa Afrika Kusini Caster Semenya amesema hatotetea taji lake la mbio za mita 800 katika mashindano ya ubingwa wa dunia baadaye mwaka huu.

Hii ni baada ya Mahakama ya Usuluhishi Michezoni yenye makao yake nchini Uswisi kuubatilisha uamuzi wa muda ambao ulimruhusu kushiriki katika mashindano ya kimataifa bila kutumia dawa za kupunguza homoni za kiume mwilini. Akizugnumzi uamuzi huo wa CAS, mwanariadha huyo amesema “ataendelea kupambana kutetea haki za binaadamu” licha ya “kusikitishwa kwake”.

Semenya anaendeleza mapambano mahakamani dhidi ya shirika la kimataifa la riadha – IAAF, kuhusu sheria ambazo zinamhitaji kutumia dawa ili kupunguza viwango vyake vingi vya homoni za kiume.

Semenya mwenye umri wa miaka 28, aliorodheshwa kisheria kuwa wa kike wakati alizaliwa na amejitambulisha kama mwanamke maisha yake yote. Alizaliwa na kromomosomu za kiume na ana hali ya kimaumbile ambayo inampa tabia za kiume na kike na kiwango cha homoni za kiume ambacho ni cha juu kuliko za kike.

Author: Bruce Amani