Agwanda mchezaji bora kwa mwezi wa pili mfululizo
Nahodha msaidizi wa Sony Sugar Enock Agwanda amekuwa mchezaji wa kwanza kuwahi kushinda mara mbili mfululizo tuzo ya mchezaji bora wa mwezi ya Sportpesa/LG/SJAK, katika ligi kuu ya Kandadna nchini Kenya baada ya kunyakua tuzo hiyo kwa mwezi wa Agosti katika uwanja wa Awendo.
Mchezaji huyo aliyewahi kuzichezea timu za Gor Mahia na Sofapaka alipata tuzo hiyo baada ya kuendeleza mchezo wake mzuri kutoka mwezi uliopita. Alipata kura nyingi na kumpiku Joe Waithira katika matokeo yaliyotolewa na kamati ya kandada ya Chama cha Waandishi wa Michezo nchini Kenya SJAK.Agwanda ambaye alijiunga na Sony katikati ya msimu akitokea Ushuru, alifunga mabao manne na kutoa assit mbili kwa wachezaji wenzake.
Mshambuliaji huyo alifunga bao lake lakwanza mwezi uliopita kupitia penalti katika ushindi wake wao wa 3-1 dhidi ya Thika United inayokabiliwa na kitisho cha kushuka daraja kabla ya kufunga bao la pekee katika ushindi wa 1-0 ugenini dhidi ya Ulinzi Stars
Kisha akafunga mabao mawili dhidi ya Kariobangi Sharks katika ushindi wao wa 2-0 na kufikisha 9 mabao yake msimu huu huku akiisaidia Sony kupanda hadi upande wa nusu ya juu ya msiamamo wa ligi baada ya kuukamilisha mwezi wa Agosti na sare ya kutofungana na Tusker.
Agwanda alipewa shilingi laki moja za Kenya, kombe na televisheni ya LG ya 49 inchi, huku timu yake inayoshikilia nafasi ya kumi kwa sasa ikipata shilingi 50,000 za ziada kutokana na mchango wake kwa mafanikio ya mchezaji huyo.
“Haukuwa uamuzi rahisi kujiunga na Sony hasa baada ya watu wengi kuona nimeisha makali. Lakini matokeo yako wazi kwa kila mmoja kuyaona. Tulikuwa katika nafasi ngumu wakati niliporudi lakini tumefanikisha lililoonekana kuwa ngumu kufanikisha”. Alisema Agwanda. Amemshukuru kocha wake kwa kuwa na Imani nae na kuongeza kuwa lengo lao ni kumaliza msimu katika nafasi ya tano bora. Kocha wa Sony Sugar Patrick Odhiambo alimpongeza mchezaji wake akisema kuwa alistahili tuzo hiyo ambayo itaipa morali timu yake.