Chelsea yalaani kauli za kibaguzi dhidi ya Tammy

179

Chelsea imepanga kuchukua hatua kali za kisheria pindi atakapopatikana mtu yeyote anayetoa maneno ya kibaguzi kwa mshambuliaji wao Tammy Abraham. Tammy Abraham, 21, tangu kumalizika kwa mchezo wa Uefa Super Cup amekuwa akitolewa maneno ya kibaguzi kupitia mtandao wa Twitter kutokana na kukosa penati ya mwisho kwenye mtanange huo baada ya dakika 120 kumalizika kwa sare ya goli 2-2 dhidi ya Liverpool ambapo Liverpool walishinda penati 5-4.

“Tumeendelea kufanya uchunguzi kugundua endapo mashabiki wa klabu yetu (Chelsea) wamehusika katika tukio hilo, endapo tutabaini kuwepo kwake tutamzuia kuingia uwanja msimu mzima ujao.

Tutaendelea kuchukua sheria kwa yeyote atakaye endelea kutoa maneno ya kibaguzi kwenye mitandao ya kijamii.” Alisema Msemaji wa Chelsea.

Kauli ya Chelsea inakuja baada ya Taasisi ya Kick It Out ambayo hujihusisha na chunguzi za kibaguzi michezoni kulalamikia tukio la ubaguzi kwa kijana huyo.

Matukio ya kibaguzi yamekuwa yakiendelea kuripotiwa kila mara licha ya kanuni kudhibiti vikali. Itakumbukwa Chelsea msimu uliopita iliwafungia mashabiki sita waliomtolea maneno ya kibaguzi winga wa Manchester City Raheem Sterling, Stamford Bridge.

Utafiti wa Kick It Out uliotolewa mwaka huu mwezi Julai ulionyesha ongezo la asilimia 43 ya kesi 274 kwa msimu uliopita sawa na kesi 192 misimu iliyopita.

Miongoni mwa mashabiki katika tukio la kibaguzi kwa Raheem Sterling alifungiwa maisha kutojihusisha na michezo.

Author: Bruce Amani