De Gea aipa Chelsea faida ya kumaliza katika nne bora

170

Manchester City wanastahili tu kushinda mechi mbili na kuhifadhi taji la Ligi ya Premier baada ya bao la kipindi cha pili la Sergio Aguero liliwapa ushindi mwembamba na usioridhisha dhidi ya Burnley uwanjani Turf Moor.

Bao la dakika ya 64 la Aguero – lililothibitishwa na mfumo wa VAR lilidhihirisha namna City walipambana na kutolewa jasho na Burnley iliyokuwa imejipanga sawasawa hasa katika safi yake ya ulinzi

City walifahamu kuwa ni ushindi pekee ambao walihitaji la sivyo wangeipa Liverpool nafasi kubwa. Ulikuwa ni ushindi wa City wa 12 mfululizo kwenye ligi

Kibarua cha nne bora?

Kindumbwendumbwe cha nafasi ya nne kimepamba moto. Kosa la kipa David de Gea lilizawadia Chelsea bao la kusawazisha wakati matumaini ya Manchester United kucheza katika Champions League msimu ujao yaliyeyuka dimbani Old Trafford.

Huku United ikiwa kifua mbele kupitia bao la Juan Mata dhidi ya klabu yake ya zamani, De Gea aliutema mpira uliotokana na kombora la Antonio Rudiger kutoka umbali wa yadi 30 na Marco Alonso akaukimbilia mpira na kuutumbukiza wavuni muda mfupi kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika. Matokeo hayo yana manaa kuwa United inabakia katika nafasi ya sita na pointi 65 moja nyuma ya Arsenal. Chelsea iko nafasi ya nne na pointi 68 mbili nyuma ya Spurs.

Jamie Vardy alifunga mara mbili wakati Leicester ilichafua ndoto za Arsenal kufuzu katika Champions League kwa kuwazaba 3 – 0 katika dimba la King Power. Leicester walipata bao la kwanza kupitia Youri Tielemans aliyefinya kichwa safi sana.

Arsenal walicheza kwa karibu saa nzima ya mechi hiyo wakiwa na wachezaji 10 uwanjani baada ya Ainsley Maitland-Niles kuonyeshwa kadi mbili za njano.

Author: Bruce Amani