Gor Mahia wahifadhi ubingwa wa ligi nchini Kenya

360

Gor Mahia Kogalo imefanikiwa kutetea tena taji la ligi Kuu ya Sportpesa ya nchini Kenya baada ya kulazimisha sare na kibonde wa ligi hiyo Vihiga United ya 1-1 katika mchezo uliopigwa Machakos.

Gor Mahia ambayo unakuwa ubingwa wao wa tatu mfululizo baada ya kuanza msimu wa 2016-2017, 2017-2018, na 2018-2019 ilikuwa inahitaji alama moja kufikia 70 ambazo zisingeweza kufikiwa na timu iliyo nafasi ya pili Bandari FC. Ni taji la 18 kwa Gor katika historia ya timu hiyo.

Ubingwa wa Gor umepitia kwenye miguu ya Charles Momanyi ambaye alifunga goli dakika ya 14 ya mchezo kabla ya Vihiga United kusawazisha goli hilo kipindi cha pili, na kufanya matokeo kuwa 1-1 mpaka dakika 90.

Baada ya mtanange Gor Mahia sasa mabingwa hao wanafikisha alama 70, alama 8 zaidi ya timu iliyo nafasi ya pili Bandari na 12 zaidi ya Sofapaka katika nafasi ya tatu.

Mbali na changamoto zilizoikabili timu hiyo za kifedha kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa kwa kushindwa kusafiri mpaka Serikali kuingilia kati haukuizuia Gor Mahia kushindwa kutetea taji la KPL kwa msimu wa tatu mfululizo.

Kutwaa ubingwa kwa Gor Mahia inaungana na Yanga Sports Club ya Tanzania katika ukanda wa Afrika Mashariki kubeba taji mara tatu mfululizo kwenye nchi husika yakiwa mafanikio makubwa zaidi kwao.

Author: Bruce Amani