Kevin-Prince Boateng ajiunga na Barcelona kwa mkopo

254

Mshambuliaji wa Ghana Kevin-Prince Boateng ameapa kuutumia vyema uhamisho wake wa kushangaza katika klabu ya Barcelona, baada ya kusaini Jumatatu mkataba wa mkopo na klabu hiyo kutoka klabu ya Sassuolo nchini Italia. Vinara hao wa La Liga wamesema katika taarifa kuwa wamekubaliana kumchukua Boateng kwa mkopi hadi mwishoni mwa msimu huu, na chaguo la kuufanya uhamisho huo kuwa wa kudumu kuanzia msimu ujao. Klabu hiyo imesema makubaliano hayo yanajumuisha kipengele cha kumnunua kwa euro milioni nane.

Kuwasili kwa Boateng mwenye umri wa miaka 31, kunatoa fursa ya nguvu kazi inayohitajika sana kwa ajili ya kusaidiana na Luis Suarez katika safu ya mashambulizi ya kikosi cha kocha Ernesto Valvarde baada ya kuondoka kwa Munir El Haddadi aliyejiunga na Sevilla.

“Barça, naja! Nna huzuni kuhama Sassuolo lakini hii ni fursa kubwa,” amesema Boateng akinukuliwa na SKY. “Lakini usiniulize kuhusu Real Madrid. Nnataka tukuangazia Barcelona na natumai kufunga bao uwanjani Bernabéu katika Clásico ijayo,” amesema Boateng

Alizaliwa nchini Ujerumani, na ni kaka wa baba mmoja wa beki wa Bayern Munich Jerome Boateng. Alihamia Serie A mwaka jana baada ya kuisaidia Eintracht Frankfurt kushinda Kombe la Shirikisho. Alifunga mabao matano katika mechi 15 msimu huu katika klabu ya Sassuolo. Boateng ametambulishwa rasmi kwa mashabiki wa Barcelona katika uwanja wa Camp Nou.

Author: Bruce Amani