Liverpool wawaongezea mbinyo vinara wa ligi Man City

145

Liverpool walipunguza pengo la uongozi wa Manchester City kileleni mwa Ligi ya Premier hadi pointi moja baada ya kuwabamiza Burnley 4 – 2 Jumapili uwanjani Anfield.

Roberto Firmino na Sadio Mane walifunga mabao mawili kila mmoja wakati timu ya Jurgen Klopp ikipambana kukusanya pointi tatu na kuwaweka katika nafasi ya pili na pointi 73, moja nyuma ya Manchester City ya Pep Guardiola.

Kichapo cha Tottenham cha tatu katika mechi nne za ligi siku ya Jumamosi kimeweka wazi kinyanganyiro cha nne bora, ambayo ni tiketi ya moja kwa moja ya kucheza Champions League.

United walipoteza mechi ya kwanza kwenye ligi chini ya kocha Solskjaer

Nao Manchester United walipata kichapo chao cha kwanza nyumbani chini ya kocha Ole Gunnar Solskjaer.

United walisafiri kwenda dimbani Emirates wakiwa katika hali nzuri baada ya kuwaduwaza mabingwa wa Ufaransa PSG katikati ya wiki katika Champions League.

Lakini msisimko wao ulikatizwa kupitia bao la Granit Xhaka na penalty iliyofungwa na Pierre-Emerick Aubameyang.

Ushindi huo wa Arsenal wa 2 – 0 umewaweka katika nafasi ya nne, pointi moja tu nyuma ya mahasimu wao wa Kaskazini mwa London Tottenham Hotspur na una maana waliwapiku Man United wakati wakilenga kurejea katika Champions League.

Awali, Eden Hazard aliinusuru Chelsea katika dakika za majeruhi aliposukuma wavuni kombora kali na kuipa timu yake pointi moja dhidi ya Wolves katika uwanja wa Stamford Bridge. Chelsea wanasalia katika nafasi ya sita, na pointi 57, lakini kocha Maurizio Sarri ana matumaini kuwa timu yake inaweza kupata tiketi ya kucheza kandanda la Ligi ya Mabingwa msimu ujao.

 

Author: Bruce Amani