Liverpool yaiangusha Bayern na kutinga robo fainali

209

Bado tu kuna aina Fulani ya ukimya katika mktaa ya Munich. Itakuwa vigumu kwa mashabiki wa Bayern Munich kusahau waliyoyashuhudia usiku wa Jumatano uwanjani Allianz Arena.

Baada ya kipyenga cha mwisho kupulizwa na taa za uwanjani kuzimwa, kisha za nje ambazo kawaida huwaka rangi nyekundu, kila mmoja alienda nyumbani akijiuliza maswali. Bayern imeondolewa katika hatua ya 16 ya Champions League. Na sio tu kuondolewa, bali walibanwa kabisa wasiweze hata kucheza kandanda lao wanalopenda.

Kuondolewa Bayern kuna maana kuwa Ujerumani haina mwakilishi katika Champions League

Aliyeongoza operesheni hiyo ni mtu anayefahamika sana katika mitaa hiyo, mtu aliyekuwa akiwasumbua sana wakati akiwa na Borussia Dortmund. Jurgen Klopp. Mabao mawili kutoka kwa Sadio Mane yaliisaidia Liverpool kutinga robo fainali kwa msimu wa pili mfululizo.

Sadio Mane aliifungia Liverpoo bao la kwanza baada ya kupata pasi ndefu kutoka kwa Virgil van Dijk na akasukuma mpira katika lango ambalo halikuwa na mtu baada ya Manuel Neuer kuchomoka mapema.

Bayern sasa walihitaji alau mabao mawili na wakapata moja kupitia bao la kujifunga kupitia Joel Matip. Hata hivyo katika kipindi cha pili, Virgil van Dijk alihakikisha kuwa Liverpool wanatinga robo fainali aliporuka na kupiga kichwa kali hadi wavuni kutokana na mkwaju wa kona wa James Milner. Mane kisha alikamilisha kazi alipofunga bao la kichwa, bao lake la 10 katika mechi 10 za mwisho.

Ushindi wa Liverpool una maana kuwa kutakuwa na wawakilishi wanne wa Premier League katika nane za mwisho kwa mara ya kwanza tangu 2009.

Author: Bruce Amani