Maafisa wa FERWAFA wachunguzwa kwa rushwa

129

Maafisa wawili wa Shirikisho la Kandanda la Rwanda – FERWAFA wanafanyiwa uchunguzi na Shirika la Upelelezi la Rwanda – RIB, kuhusiana na tuhuma za kashfa ya rushwa inayomhusisha refarii.
Maafisa wa RIB wamesema kuwa Katibu Mkuu wa FERWAFA Francois Regis Uwayezu na Kamishna wa Mashindano Eric Ruhumiriza walitiwa nguvuni Alhamisi Septemba 12.

Kashfa hiyo iligonga vichwa vya habari nchini Rwanda wakati Refarii wa Shirikisho la Kandanda la Afrika – CAF Jackson Pavaza alidai kupewa hongo na maafisa wa FERWAFA waliotaka kuyaingilia matokeo ya mchuano wa kufuzu dimba la Kombe la Mataifa ya Afrika – AFCON 2019 kati ya Rwanda na Cote d’ivoire. Gazeti la Namibia la The sun lilichapisha habari hii jumatano wiki hii, likisema muamzi huyo alisema kwamba viongozi hao walimkabidhi bahasha iliyowekwa noti na kufungwa, lakini akakataa kuichukua. Aliongeza kwamba aliripoti kwa CAF baada ya mechi hiyo.
FERWAFA ilikanusha madai hayo yaliyotolewa na refarii wa CAF, ikisema ni uwongo mtupu.

Author: Bruce Amani