Magufuli amwaga milioni 50 kwa Taifa Stars

237

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Pombe Magufuli, amewaagiza wachezaji wa timu ya Taifa Stars kwenda kupambana katika mchezo wao dhidi ya Lesotho na kurejea na ushindi.

Rais Magufuli leo alikutana na timu ya taifa na kupata fursa ya kuula nao chakula cha mchana katika Ikulu jijini Dar-es Salaam na kuwakabidhi kiasi cha shilingi millioni 50 kama mchango wake ili kufanikisha timu hiyo kuleta ushindi dhidi ya Lesotho

Katika hafla hiyo Rais Magufuli ambaye anasifika kwa msimamo na kubana matumizi hakusita kummwagia sifa kocha mkuu wa Stars Emmanuel Amunike toka nchini Nigeria

 

“Ninakuamini Amunike, ninajua utafanya vizuri na kuwasaidia vijana wetu. Lakini ninachotaka ni ushindi. Vijana wapambane na kushinda.” Alisema Rais.

Alitoa onyo kwa viongozi wa shirikisho la soka Tanzania TFF pamoja na wadau kutomwingilia kocha huyo katika utendaji wake wa kazi kama ilivyozoeleka katika siku za nyuma kwa makocha kadhaa waliofundisha soka tanzania

Lakini pia amewasisitizia wachezaji kwenda kupambana na kupeperusha vema bendera ya taifa kwani huo ndio uzalendo huku akitoa onyo kuhusi kiasi hicho cha pesa alichokitoa kwa Stars

“Fedha (Sh milioni 50), nilizotoa zitumike kwa wachezaji, nataka ushindi, mkishindwa mtazitapika kwa njia nyingine,” alisema Rais Magufuli akionyesha msisitizo kuhakikisha Stars inachomoza na ushindi katika mchezo huo dhidi ya Lesotho wa kuwania kufuzu kwa michuano ya AFCON 2019 mchezo unaotarajiwa kupigwa katikati ya mwezi Novemba jijini Maseru.

Author: Bruce Amani