Simba yapaa kileleni mwa ligi kwa kishindo na kumpa zawadi Mo

322

Wekundu wa Msimbazi Simba SC wamefanikiwa kupanda kileleni mwa msimamo wa ligi kuu ya kandanda Tanzania bara kwa kishindo baada ya kuifumua bila huruma Coastal Union ya Tanga kwa goli 8-1 katika mchezo uliofanyika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam, huku magoli sita yakifungwa na wachezaji wawili.

Simba iliyokuwa inahitaji ushindi wowote kupanda hadi nafasi ya kwanza iliwachukua dakika 11 tu kuandika goli la kwanza kupitia kwa mshambuliaji raia wa Uganda Emmanuel Okwi aliyekuwa mwiba katika mchezo huo. Goli hilo liliipa Simba nguvu ya kupata goli lingine ambalo Okwi alilifunga pia.

Coastal Union “Wagosi wa Kaya” walijipapatua wakapata goli moja kupitia Raizin Hafidh licha ya mvua ya magoli kuendelea kumiminika juu yao kama wamesimama.

Baadae Mnyarwanda Meddie Kagere alifanikiwa kufunga goli tatu (hat trick) inayomfanya kufikisha mabao 20 msimu huu katika ligi kuu akifikia rekodi ya mabao 20 ya Okwi msimu uliopita lakini akibakiza bao moja kufikia idadi ya mabao 21 aliyofunga Amissi Tambwe msimu wa 2015/16 akiwa mfungaji bora.

Kwa upande wa Okwi, mabao hayo 14, naye amemfikia nahodha wake John Bocco aliyekuwa benchi katika mechi ya leo akishuhudia ‘vijana wake” wakiwagaragaza Wagosi wa Kaya.

Mabao mengine yalifungwa na Hassan Dilunga na Cleotus Chama raia wa Zambia na kuifanya Simba iandike ushindi huo mnono zaidi kwa msimu huu.

Hii si mara ya kwanza Coastal Union kufungwa idadi hiyo ya magoli kwani Klabu ya Yanga imewai kuifunga timu hiyo goli 8-0.

Kwa ushindi wa leo, Simba imefikisha pointi 81 na kupaa kileleni ikiwaacha Yanga wenye pointi 80 waliokuwa wamekaa kileleni kwa muda mrefu zaidi.

Yanga wamecheza 34 huku Simba wakiwa wamefikisha mechi 31 baada ya kucheza mechi yao ambayo wametoa kipigo kikali kwa Wagosi wa Kaya.

Author: Asifiwe Mbembela