Timu ya Pro Piacenza ya Italia yafungwa 20 – 0

107

Kuna mashabiki waliokuwa na wikiendi mbaya kutokana na matokeo mabaya ya timu wanazoshabikia lakini kama unadhani hali yako ilikuwa mbaya sana, basi tafakari yaliyowakuta wachezaji wa timu ya Italia ya Pro Piacenza.

Timu hiyo ya ligi ya Italia ya Daraja la tatu Serie C walizabwa mabao 20 – 0, yaani ishirini kwa sifuri dhidi ya mahasim wao wa kwenye ligi Cuneo, Jumapili.

Kipindi cha kwanza kilikamilika wakiwa nyuma 16 – 0 huku mchezaji wa Cuneo Hicham Kanis akitia kimiani mabao sita kabla ya kipindi cha mapumziko, na mshambuliaji mwenzake Edouardo Defendi akitikisa nyavu mara tano

Timu hiyo inayoburura mkia katika ligi daraja la tatu nchini Italia, ipo katika matatizo makubwa ya kifedha. Walipokonywa point inane mapema msimu huu na inaripotiwa wameshindwa kuwalipa wachezaji wake tangu Agosti – na hivyo kusababisha wengi wa wachezaji wao wa kikosi cha kwanza kujiuzulu.

Pia walishindwa kucheza mchuano wao wowote kati ya mitatu iliyopita kabla ya mechi ya Jumapili waliyozabwa, na kama wangesusia kucheza dhidi ya Cuneo, ina maana wangetimuliwa katika ligi ya Serie C. kwa hiyo walianza mechi hiyo na matineja saba. Bila kuwa na benchi la makocha, ilibidi nahodha Nicola Cirigliano achukue majukumu ya ukocha.

Gabriele Gravina, rais wa Chama cha Kandanda cha Italia aliyaelezea matokeo hayo ya Jumapili kuwa ni “matusi kwa mchezo wa kandanda.”

Author: Bruce Amani