Ushindani wa Yanga na Simba wazinufaisha klabu hizo

540
Waswahili husema “Usijisifu una mbio, msifu anayekukimbiza” usemi huu waweza sadifu sawa na kile kinachoendelea nchini Tanzania kwa vilabu vikongwe kwa maana ya Simba SC na Yanga SC
Simba imefikia mafanikio makubwa sana katika soka la nchi hii hata haitaji taaluma yoyote kutambua hilo, kuanzia kwenye uwekezaji, maandalizi ya timu hiyo hata usajili pia imepiga hatua kubwa sana.
Kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika sio jambo la kuchukuliwa kiwepesi hata kidogo, kuzifunga AS Vita, Al Ahly ni jambo kubwa pia.
Mafanikio hayo kwa kiasi kikubwa yameletwa na yule anayeikimbiza bila kujali anamfuata kwa nyuma au wako sawa. Simba ilitia bidiii kufanya vizuri ili kuondokana na aibu kutoka kwa mtani wao Yanga.
Aidha upande wa Yanga pia baada ya kuona inaikimbiza Simba ambayo inaonekana kuwa mbali kimaendeleo, ilifafanya mbinu ambazo zinaipaisha kwa sasa. Kuanzia upatikanaji wa uongozi mpya baada ya misukosuko mingi, namna ya kuendeshwa timu hiyo. Inakukumbusha kumtazama anayekukimbiza bila kuangalia ni nani.
Usichoke, makala haya yanaangalia namna ushindani baina ya timu hizi mbili unavyoleta faida ndani ya vilabu na kukua kwa soka la nchi. Kwa maana huwezi ukazungumzia mafanikio ya soka nchini bila kuzigusa klabu hizo.
UTAMBULISHAJI WA JEZI
Msimu wa 2019/20 umeshuhudia utambulishaji wa jezi wenye ubora zaidi tofauti na miaka mingine. Kuanzia kwenye matangazo mpaka siku yenyewe ya utambulisho. Haikuwa kawaida kuona uzinduzi wa jezi kuteka mijadala ya kwenye mitandao ya kijamii hasa katika mauzo lakini sasa imewezekana.
Mauzo ya jezi pia yamefanywa tofauti.
Haijatokea kama ajali bali kila klabu zimekuwa zikitamani kuleta kitu bora zaidi ya mshindani wake. Ushindani wa bila kutambua umepelekea kuwavutia zaidi wanunuaji kwa maana ya mashabiki wa timu husika kwa misingi ya ubora wa bidhaa.
USAINISHWAJI WA MIKATABA
Yanga imeingia makubaliano ya kimkataba na Kampuni ya GSM kwa ajili ya kutengeneza na kusambaza vifaa vya kimichezo vyenye nembo ya Yanga. Ni mkataba mnono zaidi ya milioni 300 zimewekwa mezani. Kandarasi hii imepelekea mpinzani kushituka na kisha kujibu mapigo.
Baada ya Yanga, Simba nayo ikaingia kwenye mkataba na Kampuni ya Uhlsport kwa ajili ya kutengeneza vifaa vya michezo kwa mkataba wa milioni 600 kwa miaka miwili. Simba pia imeingia kandarasi na benki ya Equity kwa ajili ya kutengeneza kadi za Wanachama jambo ambalo naamini Yanga pia inaweza ikalichukua kwani lina faida kubwa.
KUFANYIKA KWA MATAMASHA
Miaka 10 iliyopita Simba ilianzisha tamasha liloitwa Simba Day, lililokuwa na kusudi ya kutambulisha wachezaji na kikosi cha Wanamsimbazi hao.
Baada ya miaka hiyo, Yanga wakaanzisha kitu kama hicho kinachoenda kwa jina la “Wiki ya Mwananchi” kusudi na lengo likabaki kuwa lile lile licha ya kuongeza ubunifu kidogo.
UJAZAJI WA UWANJA.
Hivi sasa kuna kampeni ya kiushandani ya chini kwa chini inayopita kuhamasisha mashabiki wa timu husika (Yanga na Simba) kujaza uwanja wa taifa huku wakivalia uzi njano au mwekundu. Kampeni hii hupelekea uwanja kujaa na unapelekea timu kupata fedha kupitia ununuaji wa jezi sambamba na ada ya mlangoni.
Aina hii ya ushindani katika siku za karibuni imekuwa chachu kubwa katika kuzijenga timu hizi hasa kiuchumi.
Ushindani huo ambao umekuwa ukifanyika katika siku za hivi karibuni nchini hasa Simba na Yanga naamini unafaida kubwa na nyingi ambazo endapo umakini utaongezeka katika kuandaa vitu vyote kiustadi na weledi, timu zitakuwa na uwezo wa kujiendesha hata zenyewe kwa sababu zitakuwa zinavuna faida kutoka kwa mashabiki wao.
Hali kadhalika ushindani huo mfano usainishwaji wa mikataba, uzinduzi wa jezi vinaweza kuleta fedha nyingi sana.

Author: Asifiwe Mbembela