Yanga kukosa huduma ya Makambo dhidi ya Mwadui

404

Klabu ya Yanga kushuka uwanja wa taifa kesho Jumanne Januari 15 saa 1 kamili usiku kucheza dhidi ya Mwadui FC ukiwa ni muendelezo wa ligi kuu Tanzania bara ambapo itaingia katika mtanange huo bila huduma ya mshambuliaji kinara wa magoli katika ligi hiyo Heritier Makambo.

Yanga ilikuwa katika mapumziko ya takribani wiki mbili kwa baadhi ya wachezaji wa kikosi cha kwanza, tangu ilipomaliza mchezo dhidi ya Mbeya City na kuibuka na ushindi wa goli 2-1. Makambo alienda kwao Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na bado hajarejea Tanzania.

Akizungumza na Wanahabari msemaji wa klabu hiyo Dismas Ten amesema “Makambo alienda nyumbani kwao (Congo) kwa mapumziko maalum aliyopewa na kocha kama wachezaji wengine walivyoenda ingawa bado hajarejea hatuwezi kujua amekumbwa na nini huko lakini siku mbili hizi simu yake haipatikani” alisema Ten.

Yanga ipo nafasi ya kwanza kwa alama 50 katika michezo 18 itakuwa inahitaji alama 3 ili kuendeleza wigo wa alama kwa timu zinazofuata chini.

Aidha, Mwadui FC ipo nafasi ya 11 michezo 21 ikiwa imekusanya alama 24 itahitaji kuibuka na ushindi ili kujiweka katika mazingira salama ya kutoshuka daraja lakini pia kuendeleza rekodi nzuri ambayo mara kadhaa wamekuwa wakiionyesha wanapocheza na Simba au Yanga.

Author: Bruce Amani