Yanga yawafungia kazi Township Rollers, kurekebisha mapungufu

248

Yanga SC wamewasili salama Kilimanjaro waliokoenda kuweka kambi ya wiki mbili ya kujiwinda na mchezo wa mkondo wa pili dhidi ya Township Rollers ya Gaborone Botswana, mchezo unaotegemewa kupigwa mwishoni mwa mwezi Agosti. Yanga inaingia kambini kwa wiki hizo mbili ikijiweka sawa katika mazingira mengi ambayo awali hayakuwa sawa kabla ya kuanza safari ya Botswana.

SEHEMU YA KWANZA NGAZI YA KOCHA

Yanga ilikuwa chini ya kocha msaidizi katika maandalizi ya msimu wa 2019/20 wa TPL, FA, na Ligi ya Mabingwa chini ya kocha msaidizi Noel Mwandila jambo lililozorotesha juhudi na mbinu za kocha. Kuchelewa kwa kocha Zahera kuna athari katika muda kwa sababu alipofika kwa kuchelewa analazimika kuziingiza mbinu zake kwa haraka kwa kiasi fulani amefaulu mfano Mwinyi Zahera ni muumini wa mpira wa kasi kupitia mawinga hilo linaonekana.

KUWARUDISHA WACHEZAJI UWANJANI

Wachezaji wengi waliosajiliwa msimu huu Yanga walikuwa hawana utimamu wa kutosha pindi wanajiunga na timu hiyo. Maybin Kalengo (Zambia) alikuwa na majeraha ya mda mrefu hata mazoezi ya Morogoro hakufanya mazoezi kwa asilimia 100. Sadney Ukrihob, Lamine Moro, Raphael Daud ni wachezaji waliotegemea zaidi mazoezi ya mtu na sio timu kwa sababu kipindi hicho hawana timu, hivyo waliingia wakihitaji mazoezi na muunganiko wa timu, Daud akisumbuliwa na majeraha sasa ndio anarudi.

David Mulinga “Falcao”, usajili wa siku ya mwisho. Mwalimu Zahera amekuwa akitumia mda wa ziada kumnoa strika huyo.

KUTAFUTA MUUNGANIKO WA TIMU

Wataalamu wa soka wanakubaliana kwamba kuwa na kipaji pekee haitoshi kuwa mchezaji bora bali ni namna ipi unatumia kipaji chako kushirikiana na wenzako kuleta mafanikio ya timu kwa sababu soka ni mchezo wa timu.

Limekuwa tatizo kubwa kwa kocha Mwinyi Zahera tangu awasili jangwani baada ya mapumziko, anaonekana bado anatafuta muunganiko ndiyo maana hana kikosi cha kwanza (First XI). Muunganiko huo ndiyo unaofanya kujua mchezaji fulani nikipiga pasi hii ataikuta ama kuumiliki mpira namna fulani.

KUPATA MECHI ZA USHINDANI NA HALI YA HEWA

Tofauti na mechi za awali kule Morogoro, hivi sasa Yanga itacheza michezo miwili inayoonyesha wanataka nini. Itacheza na Polisi Tanzania na AFC Leopards ya Kenya timu zote zipo kwenye maandalizi ya msimu ujao. Hili linakupa picha ya kutafuta ushindani.

Pili ni hali ya hewa na Botswana hivi sasa haina utofauti mkubwa na mikoa ya Arusha, na Kilimanjaro. Hivyo kuwa sehemu hiyo kutawapa utulivu pamoja na kuzoea hali ya hewa ya eneo la vita.

Kocha Mwinyi Zahera amejitapa kwenda kufanya maajabu kwenye mechi ya marejeano licha ya kuwa na mzigo mzito wa kurudisha goli. Hata hivyo kurejea kwa kitasa Kelvin Yondani, Juma Abdul na Andrew Vicente “Dante” imekuwa ngao kwa Wanayanga kufanya vizuri.

Author: Bruce Amani