Zidane apata kipigo cha kwanza tangu aliporejea Madrid

149

Valencia wameyapiga jeki matumaini yao ya kumaliza katika nafasi nne za kwanza kwenye ligi kwa kupata ushindi wa 2 – 1 dhidi ya Real Madrid. Ni kichapo cha kwanza cha Zinedine Zidane tangu aliporejea katika klabu hiyo kama kocha mkuu.

Valencia waliingia kwenye mechi hiyo wakiwa katika nafasi ya saba lakini walifahamu kuwa wangeweza kupunguza mwanya dhidi ya nambari nne Getafe baada ya sare yao ya 1 – 1 na Espanyol Jumanne.

Walipata bao la kwanza mbele ya mashbabiki wao dakika kumi kabla ya kipindi cha mapumziko kupitia mchezaji Goncalo Guedes. Valencia kisha wakaongeza la pili katika dakika za mwisho kupitia bao la kichwa la Ezequiel Garay.

Karim Benzema alifunga bao dakika za majeruhi kupitia kichwa lakini hakukuwa na muda wa Madrid kupata bao jingine. Valencia sasa wamesonga hadi nafasi ya tano, pointi moja nyuma ya Getafe. Real wako nafasi ya tatu.

Author: Bruce Amani