Zifahamu rekodi mbaya za Yanga Kombe la Shirikisho FA

688

Je wajua, tangu msimu wa 2015/2016 Yanga haijawai kucheza Uwanja wa nyumbani robo fainali ya FA na mechi zote imepoteza?

Jumamosi Machi 30, 2019 Klabu ya Yanga itacheza robo fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Alliance FC kutoka Mwanza katika Dimba la CCM Kirumba.

Kuelekea mchezo huo Amani Sports News inakusogezea rekodi za Yanga kwenye FA.

Huu ni msimu wa tatu mfululizo kwa Yanga kucheza robo fainali kiwanja cha ugenini tangu ilipofanya hivyo mara ya mwisho mwaka 2016 ilipocheza dhidi ya Ndanda.

Msimu wa 2016/17 ilicheza dhidi ya Mbao FC ya Mwanza katika uwanja wa CCM Kirumba, wakati msimu uliofuata kwa maana ya 2017/18 ilicheza dhidi ya Singida United uwanja wa Namfua, msimu huu pia Yanga itacheza dhidi ya Alliance FC kutoka Mwanza dimba la CCM Kirumba.

Katika misimu yote ambayo Yanga imekuwa ikicheza ugenini imepoteza michezo yake na kushindwa kufika nusu fainali.

Aidha, mbali na kupoteza michezo pia ilikuwa inatolewa na timu zilizopanda daraja msimu husika, ilitolewa na Mbao iliyokuwa imepanda daraja, ikatolewa na Singida vivyo hivyo, je msimu huu Yanga itaendeleza rekodi mbaya dhidi ya timu zilizopanda daraja?.

Timu zilizoiondosha Yanga zilifika hatua ya fainali licha ya kushindwa kutwaa ubingwa, je safari ya Alliance itakuwa sawa na Mbao ama Singida United?

Kila timu hivi sasa ziko katika maandalizi moto moto ambapo Alliance imeweka kambi nchini Rwanda kujiwinda na mchezo huo wakati Yanga ikisalia Dar es Salaam.

Akizungumzia maandalizi ya kikosi, Msemaji wa Yanga Dismas Ten amesema timu inaendelea vizuri, ambapo kuna wachezaji waliorejea wakimaliza kuuguza majeraha akiwemo Juma Mahadhi aliyekosekana kwa mda mrefu.

Michezo yote miwili ya ligi kuu ya kandanda Tanzania bara (TPL), Alliance ilikubali kupoteza michezo hiyo.

Yanga imefunga goli 5 wakati Alliance akifunga goli 1 tu, katika mtanange uliofanyika CCM Kirumba. Je rekodi hii Alliance itaipindua na kuibuka na ushindi?.

Author: Asifiwe Mbembela